Siku ya Hedhi salama: Kufanya hedhi kuwa jambo la kawaida kufikia mwaka wa 2030

Aisha aliogopa na kuchanganyikiwa alipoona doa la damu kwenye sketi yake. Alikuwa msalani shuleni, akijiuliza kama hiki ndicho walichojifunza darasani kuhusu miili ya wasichana. Akiwa bado na wazo hilo akilini, kuna mtu alikuwa akigonga mlango, akitaka kutumia choo. Aisha alitamanin kuondoka na kurudi darasani, lakini alikumbuka jinsi Chausiku alivyokuwa amedhihakiwa na wavulana mwaka uliopita wakati alipopopata hedhi yake ya kwanza wakiwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Aisha alibaki tu pale amesimama, bila kujua la kufanya!

Hedhi ni utaratibu wa kawaida wa kibiolojia ambao huandaa mwili wa mwanamke kwa ajili ya ujauzito kila mwezi. Kwa kawaida hedhi huanza kati ya umri wa miaka 8 na 15 na inaweza kuacha kati ya miaka 45 na 55 au zaidi. Kwa wastani, mzunguko wa hedhi huchukua siku 28, lakini kinaweza kutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, na kipindi cha hedhi huwa kwa muda wa siku 2 hadi 5. Kipindi cha hedhi kinaweza kusababisha dalili fulani kama vile maumivu ya tumbo, tumbo kujaa gesi, mabadiliko ya hisia, na chunusi. Dalili hizo ni za kawaida na hazina madhara, lakini watu wengine wanaweza kupata dalili kali zaidi zinazohitaji matibabu.

Hedhi salama ni muhimu katika kuboresha afya kwa kuzuia maambukizi, kupunguza harufu mbaya na kufanya wanawake/wasichana wajisikie vizuri. Baadhi ya changamoto zinazohusiana na afya na hedhi salama (MHH) nchini Tanzania, ni pamoja na ukosefu wa taulo za keki safi na za bei rahisi; Utafiti uliofanywa na AAPH huko Tanga uliopewa jina “Harnessing longitudinal data and digital technologies to improve adolescent health in Tanzania” ulionyesha kuwa zaidi ya theluthi moja (35%) ya wasichana walikuwa wakitumia kitambaa au vipande vya nguo, na takriban 20% ya wasichana walikosa shule kwa sababu ya ukosefu wa bidhaa za usafi na 12% kwa sababu ya hofu ya kuvuja.  Tatizo jingine ni kwamba hedhi inachukuliwa kuwa jambo lisilo la kawaida katika jamii zetu, na hivyo ni vigumu kwa wasichana kutafuta msaada na wanaona aibu wanapokuwa katika hedhi. Pia ukosefu wa mfumo wa msaada kwa wasichana / wanawake wakati huu; takriban 15.9% ya wasichana waliripotiwa kukosa shule kwa siku 1-2 kwa sababu ya hedhi, haswa kwa sababu ya maumivu, ukosefu wa vyumba vya kubadilisha nguo, ukosefu wa vifaa safi na vinavyofaa katika maliwato, na ukosefu wa maji, lakini hakukuwa na mfumo elekezi wa kuwasaidia ili kulipia masomo yaliyokosa[1] [2].

Ili kuendeleza MHH, tunaweza kuchukua hatua kadhaa: kuelimisha wanajamii juu ya ukweli na masuala ya MHH, kuhakikisha taulo za kike za bei nafuu na zenye ubora zinapatikana, kukabiliana na kubadilisha kanuni na imani za kijamii zenye madhara kuhusu hedhi, na kuboresha vifaa vya maliwato na ugavi wa maji.

Katika Siku ya Hedhi salama, tunakusudia kumaliza ukimya na aibu kuhusu hedhi, kuongeza ufahamu kuhusu vizuizi vya afya na hedhi salama, na kukuza upatikanaji wa bidhaa za hedhi, elimu na vifaa. Lengo letu ni kuunda ulimwengu ambapo hedhi haizuii uwezo wa mtu yeyote, hebu tufanye hedhi kuwa jambo la kawaida katika maisha ifikapo mwaka 2030, kwa afya bora ya umma. [3]